MFUMO UNGANISHI WA TAARIFA ZA ARDHI MTANDAONI WAZINDULIWA
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imezindua mchakato wa kujenga mfumo unganishi wa taarifa za ardhi kwa njia ya mtandao wa inteneti (ILMIS), ambao unatarajiwa kuwa msaada mkubwa katika kutatua migogoro ya ardhi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe. William Lukuvi akiwa amemaliza tukio la Uzinduzi wa Miradi ya upatikanaji wa picha za anga (Basemap) na mfumo unganishi wa taarifa za Ardhi (ILMIS) . Wanaoshuhudia pamoja naye; Kulia kwake ni Waziri nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mhe. George Simbachawene, kushoto kwake ni Naibu wake; Mhe. Angeline Mabula na pembeni kabisa ni Katibu Mkuu wake; Dk. Yamungu Kayandabila katika Ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa Mwl. J.K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Mfumo huo ambao pia utahusisha upigaji picha wa jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuandaa ramani ya jiji, unatarajia kuanza kufanya kazi wilaya ya Kinondoni, kisha wilaya zote za mkoa wa Dar na baadaye katika kanda zingine. Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo, Mhe. Lukuvu alisema, “mfumo huu utatuwezesha kuwa na uhakika wa kupata kwa haraka taarifa za wamiliki halali wa viwanja na kupunguza au kumaliza migogoro inayohusu viwanja kutolewa mara mbili.” Aidha amefafanua kuwa, chini ya mfumo huo haitakuwa rahisi kwa mtu kughushi nyaraka za umiliki wa viwanja, ambavyo nyaraka zake zimepotea na kutambua maeneo yaliyopagwa kwa shughuli maalum ili kudhibiti udanganyifu katika sekta ya ardhi.
“Mfumo huu, utatoa uhakiki wa usalama wa nyaraka mbalimbali za sekta ya ardhi na kuwezesha ufuatiliaji wa matumizi bora ya ardhi na chini ya utekelezaji wa miradi huu, wizara yangu itaboresha huduma za upimaji kwa kila kanda”,aliongezea. Naye Katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk. Yamungu Kayandabila, amesema, “serikali imeamua kujenga mfumo huo ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya taarifa za sekta ya ardhi ambalo limesababisha uwepo wa hitaji la mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu za ardhi na mfumo wa kufuatilia pango la kodi ya ardhi.”
MFUMO UNGANISHI WA TAARIFA ZA ARDHI MTANDAONI WAZINDULIWA
Reviewed by Elimutehama
on
01:32:00
Rating:
No comments: