NAULI ZA MABASI NA DALADALA KUANZA KULIPWA KIELEKTRONIKI KUANZIA MWAKANI



Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imetangaza kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ukataji wa tiketi za mabasi na daladala kwa njia ya kielektroniki.

Mkurugenzi wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema jana kuwa mfumo huo wa tiketi za daladala kwa njia ya elektroniki, utaanza kutumika Januari mwakani.Lakini, aliongeza kuwa kuanzia Desemba mwaka huu, watafanya mpango huo kwa majaribio kwa mabasi yaendayo mikoani.

“Kwa sasa tumeanza mpango huo kwa majaribio kwa daladala za kampuni ya Christian, Desemba tutaenda kwa mabasi ya mikoani na Januari mwaka kesho, mfumo huo utaanza kwa mabasi na daladala zote,” alisema Kahatano. Alitangaza mfumo huo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi kwa madereva, ambayo inahusisha usafi wa mwili, mavazi na mabasi uliofanyika katika stendi ya Makumbusho, Dar es Salaam. Katika kampeni hiyo, madereva na makondakta watajishonea wenyewe sare zao na sio wamiliki wa magari.

Kahatano alisema chini ya mfumo wa ukataji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki, utamfanya mmiliki wa basi kujua mapato yake halisi kwa siku na hivyo atawalipa wafanyakazi wake mshahara na Serikali itapata kiwango sahihi cha kodi. Kwa sasa ukataji wa tiketi za mabasi na ule wa daladala, unafanywa kwa tiketi zilizochapishwa.

Alisema kutokana na mfumo huo mpya, dereva haruhusiwi kumlipa mmiliki hesabu ya kila siku kama wanavyofanya sasa.Badala yake, mmiliki ndiye atatakiwa kumlipa dereva na kondakta wa gari lake mshahara kila mwisho wa mwezi.

Alisema ili malipo hayo yaweze kufanyika ni lazima madereva waajiriwe rasmi na walipwe chini ya mfumo wa ajira.“Kwa hiyo dereva na mmiliki wataingia mkataba wa ajira tofauti na sasa hivi hakuna mkataba wowote kati ya tajiri na wafanyakazi wake, badala yake wanakubaliana tu kwamba hesabu ya siku ni kiasi fulani cha fedha na dereva anahangaika kukitafuta,” alisema Kahatano.

Kuhusu sare za madereva, alisema kwamba ndani ya wiki mbili madereva wa wilaya ya Kinondoni, wote wanatakiwa wawe wamebadili sare zao na kushona ambazo wamekubaliana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Kuhusu kuanza kutumika kwa mfumo wa kutoza nauli kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, Mwenyekiti wa daladala wa vituo vya Simu 2000, Tegeta na Bunju, Stanley Kijave,alisema mfumo huo utaleta ahueni kwa dereva na kondakta wa daladala kwa sababu wataingizwa kwenye mfumo wa ajira rasmi.

“Kwa hiyo na sisi madereva tutaingizwa kwenye mifuko ya pensheni.” Kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi cha Madereva, Shaban Mdemu alisema utaratibu wa kuwaajiri madereva kama chama wamekuwa wanaulilia na akashukuru Serikali kuja na utaratibu huo mpya.
NAULI ZA MABASI NA DALADALA KUANZA KULIPWA KIELEKTRONIKI KUANZIA MWAKANI NAULI ZA MABASI NA DALADALA KUANZA KULIPWA KIELEKTRONIKI KUANZIA MWAKANI Reviewed by Elimutehama on 04:21:00 Rating: 5

No comments:

WASILIANA NASI KUPITIA

Barua pepe/Email:123shadhili@gmail.com
copyright@2016. Theme images by enot-poloskun. Powered by Blogger.